Wanachama watatu wa
chama cha upinzani nchini Gambia wamefariki baada ya kukamatwa na
kuzuiliwa na serikali wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa umesema.
Kupitia taarifa, Katibu Mkuu wa UN Ban Ki-moon amesema amesikitishwa na kifo cha mwanachama wa chama cha United Democratic Party (UDP) Solo Sandeng na wanachama wenzake wawili.
Ameomba kuwe na uchunguzi huru kuhusu vifo hivyo pamoja na kuachiliwa bila masharti kwa wanaharakati hao wengine wanaozuiliwa.
"Katibu mkuu amesikitishwa sana na kutumiwa kwa nguvu kupita kiasi katika kuwakamata na kuwazuilia waandamanaji waliokuwa wakiandamana kwa amani,” taarifa hiyo imeongeza.
Kiongozi mkuu wa upinzani Ousainou Darboe alikamatwa Jumamosi pamoja na wafuasi wengine wa chama hicho waliokuwa wamekusanyika Serrekunda, karibu na mji mkuu Banjul, kuitisha kuachiliwa huru kwa watu wanaozuiliwa, pamoja na miili ya wale waliofariki korokoroni.
Kiongozi wa Gambia Yahya Jammeh ameongoza taifa hilo la Afrika Magharibi tangu 1994.
Anatarajiwa kuwania tena kwenye uchaguzi mkuu unaopangiwa kufanyika Desemba.
chanzo bbc swahili
No comments:
Post a Comment