Wednesday, 2 November 2016

Rais Mugabe Aidhinisha 'sarafu mpya' Zimbabwe

 Na Neema Dandida
 
Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametumia mamlaka ya ofisi yake kutoa dikrii inayoidhinisha matumizi ya sarafu mpya nchini humo, licha ya asasi za kiraia kusisitiza kuwa uamuzi huo ni kinyume cha sheria.
Patrick Chinamasa, Waziri wa Fedha wa Zimbabwe amesema Mugabe ametumia kifungu cha 133 cha Sheria ya Mamlaka ya Rais ya 2016, kuidhinisha matumizi ya sarafu hiyo inayoshabihiana na Dola ya Marekani na kufafanua kuwa, kwa sasa ni halali kutumia sarafu hiyo katika mabadilishano ya bidhaa na huduma mbalimbali.
  
Patrick Chinamasa, Waziri wa Fedha wa Zimbabwe.
Hata hivyo aliyekuwa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Tendai Biti, amekosoa uamuzi huo wa Mugabe na kusema kuwa ni wa kidikteta na unaokiuka katiba ya nchi.

Nchi ya Zimbabwe imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kifedha hasa baada ya kushuka thamani ya sarafu yake kuanzia mwaka 2009 na kuamua kuanza kutumia Dola ya Marekani.
Tangu kipindi hicho, mbali na Dola ya Marekani, raia wa Zimbabwe wamekuwa wakitumia sarafu zingine za kigeni kama Yuro, Yuan ya China, Pauni ya Uingereza na Rand ya Afrika Kusini.

  Maandamano dhidi ya serikali nchini Zimbabwe.

Katika siku za hivi karibuni, Zimbabwe imekuwa ikishuhudia maandamano ya wapinzani wanaomtaka Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 92 aondoke madarakani wakisisitiza kuwa ameshindwa kutatua matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira nchini humo.
                                 Chanzo Pars Taday

No comments:

Post a Comment