Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji.
Serikali
ya Norway imeipatia Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) zaidi ya Sh. bilioni 10 kwa
ajili ya kuwaongezea uwezo wa ukusanyaji mapato ya ndani ili kuondokana na
bajeti tegemezi.
Kadhalika, fedha hizo
ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalamu wa TRA kuhusu mbinu mbalimbali za
kukusanya kodi kwa makampuni ya ndani na ya kimataifa ikiwemo makampuni ya gesi
na mafuta.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika halfa hiyo, Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema fedha hizo, ambazo ni dola za
Kimarekani milioni tano, zimetolewa kuisaidia TRA katika jitihada zake za
kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Alisema lengo la
kufanya hivyo ni kuongeza mapato ili kusiwapo na ukwepaji kodi, kuimarisha
mpango wa ukusanyaji wa kodi na kuielimisha wananchi umuhimu wa kulipa kodi
bila kushurutishwa.
Dk. Kijaji
alisema wamefurahishwa na msaada huo kutoka kwa serikali ya Norway
kuendelea kuwasaidia kwa kuwa wanataka kuondokana na bajeti tegemezi na kuanza
kujitegemea.
Alisema ili kuondokana
na suala hilo wanatakiwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato nchini ili kuwa na
bajeti yao.
Aidha, alisema tayari
jambo hilo wameanza kulifanyia kazi ndiyo maana katika kipindi cha miezi mitatu
iliyopita makusanyo ya kodi yameongezeka na kwamba mikakati yao katika kipindi
cha mwaka mmoja ni kukusanya Sh. Trilioni 22
Alisema kwa sasa kuna
mpango mkakati wa kuwafikia walipakodi ikiwa sehemu ya harakati za kuondokana
na bajeti tegemezi.
“Uwezo tunao na mipango
yetu ni kuongeza ukusanyaji wa mapato kufikia Sh. trilioni 22 kwa mwaka ambayo
ni sawa na bajeti ya Tanzania,” alisema
Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje nchini Norway, Tone Skogen, alisema msaada huo unalenga kuboresha
maendeleo ya biashara nchini na kuvutia uwekezaji ili kufanikisha maendeleo
yaliyowekwa kwenye dira ya maendeleo
“Ni furaha yangu
kuzindua ukurasa mpya wa ushirikiano wa masuala ya kodi kati ya Tanzania na
Norway ,” alisema Skogen,
Skogen alisema
ushirikiano kati ya Tanzania na Norway kwenye masuala ya ukusanyaji wa mapato
ya ndani umeimarika.
Naye Kaimu Kamishina
Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alisema lengo la mamlaka yake ni kuimarisha uwezo
wa wataalamu wao katika kukagua maeneo makubwa hususan gesi asilia na
madini ili kuwahesabia kodi wanazotakiwa kulipa.
Alisema hawakuwa na
kitengo cha kodi za kimataifa, hivyo Norway imewasaidia kuwawezesha kuyabaini
kampuni ambazo hazilipi kodi
Kidata alisema awali
walipatiwa dola milioni 3 kwa ajili ya kusaidia uwezo wa ukusanyaji wa mapato
ambapo msaada huo uliishia kwa mwaka jana.
chanzo ipp media
No comments:
Post a Comment