waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji Charles mwijage |
Serikali imesema
itatoa kipaumbele kwa wawekezaji wa viwanda wazawa ili kuimarisha uchumi wa
nchi kwa kuweka mkazo kwenye viwando vidogo na vya kati.
Akizungumza hayo wakati wa ufunguzi
wa Mkutano Mkuu wa 16 wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema ujenzi wa viwanda utasaidia
kuzalisha ajira kwa zaidi ya asilimia 40 ya vijana nchini kama ilivyoahidiwa na
CCM katika Ilani ya uchauzi.
“Kuna msemo wa kikwetu unaomaanisha
huwezi kumlisha mtoto wa Kware ili anenepe na kumwacha wa kuku, hivyo siwezi kumwacha
mzawa nyumbani kwangu nikampa kipaumbele mgeni,” alisema Mwijage.
Alisema umefika wakati muafaka kwa
sekta binafsi kutumia nafasi zilizopo kuwekeza na kwamba serikali inahitaji
ushauri kutoka kwa wafanyabiashara na itasaidia kuweka mazingira mazuri kwa
ajili ya uwekezaji wa wazalendo.
‘’Tukisema ukweli ni kwamba kuna
baadhi ya sera zilikuwa mbovu na ndizo zilikuwa kikwazo katika kukuza viwanda,
hivyo wafanyabiashara waache kulalamika bali waseme ili serikali ifanyie kazi
mawazo yao kwani Rais (John) Magufuli yuko tayari kufuata ushauri na kutekeleza
ili kufikia azma yake ya viwanda.
Alisema kwa kipindi kifupi Watanzania
wataona bei ya sukari kuwa ni kubwa lakini amelifanyia kazi na viwanda vya
sukari vitajengwa vya kutosha nchini kwa kuwa baadhi ya wawekezaji wamejitokeza
ili kujenga viwanda hivyo. Aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu kwa sababu
serilkali imeamua sukari yote itakayouzwa itakuwa ya hapa nchini ili
kuwanufaisha wawekezaji na wakulima wa miwa.
Alisema baada ya sukari, serikali sasa
inaangalia uzalishaji wa mafuta ya kupikia kutokana na mawese yanayozalishwa
nchini na kwamba ulimaji wa michikichi utaongezwa kwa kuwa kuna mpango wa
kujengw kiwanda kikubwa cha kutengeneza mafuta mkoani Mtwara.
Mwijage alikiri kuwa viwanda vingi
vilivyokuwa vikimilikiwa na serikali, viliuzwa kwa bei ya kutupwa,
lakini akasema serikali inapitia kiwanda kimoja baada ya kingine na kama
vitakuwa havifanyi kazi kama ilivyotakiwa, vitachukuliwa na kurejeshwa kwa
wananchi.
“Nimemwambia mmiliki wa kiwanda cha
Bora kama kitakuwa hakizalishi viatu ifikapo mwezi wa tisa basi tutakichukua
kwani hata bei aliyonunulia haifikii bei ya kiwanja Pugu Road,” alisema.
Kw aupande wake Mwenyekiti wa TPSF,
Dk Reginald Mengi alimpongeza Rais Magufuli kwa kuthamini sekta binafsi nchini
na kukusanya kodi na kuondoa ufisadi na rushwa, hivyo kufanya wafanyabiashara
kujisikia raha wanapolipa kodi serikalini.
“Sekta binafsi imefarijika kwa
jitihada na spidi (kasi) ya serikali kurejesha utawala wa sheria, haki na
uwajibikaji katika sekta ya umma na kutoa uamuzi ambao unakuza biashara na
uwekezaji,” alisema.
Chanzo
ipp media
No comments:
Post a Comment