Wednesday, 2 November 2016

Uzalishaji mafuta warejea katika hali yake ya kawaida nchini Nigeria

Na Neema Dandida
Waziri wa Mafuta wa Nigeria amesema kuwa, uzalishaji mafuta umerejea katika hali yake ya kwaida nchini humo.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Emmanuel Ibe Kachikwu akisema hayo jana na kuongeza kuwa, uzalishaji mafuta nchini Nigeria umefikia mapipa milioni mbili na laki moja kwa siku jambo ambalo linaonesha kufikiwa kiwango chake cha kawaida cha kabla ya kuharibiwa taasisi za kuzalisha mafuta za nchi hiyo.

Wiki chache zilizopita, serikali ya Nigeria ilifanya mazungumzo na kundi la waasi wa Niger Delta la kusini mashariki mwa nchi hiyo kwa upatanishi wa mashirika ya kigeni na jeshi la polisi kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi tatizo la ukosefu wa amani ambalo limeathibiri vibaya eneo hilo kwa muda mrefu sasa.

Uharibifu wa mabomba ya mafuta mara nyingi hufanyika kwa lengo la kuiba mafuta hayo, na jambo hilo limekuwa la kawaida sana nchini Nigeria, ambayo ni mzalishaji mkuu wa mafuta ghafi barani Afrika.

Waziri wa Mafuta wa Nigeria amesema, mazungumzo baina ya serikali na waasi yamekuwa na mafanikio makubwa. Amesema, malengo ya mwaka 2017 ya nchi yake ni kumaliza kabisa vitendo vya uharibifu vinavyofanywa na makundi mbalimbali ya nchi hiyo.
Sehemu kubwa ya mafuta ghafi ya Nigeria yanazalishwa katika eneo la Niger Delta la kusini mashariki mwa nchi hiyo. 

Asilimia 80 ya bajeti ya Nigeria inategemea uuzaji nje mafuta ghafi ya nchi hiyo.
                             chanzo pars today

No comments:

Post a Comment