Wednesday, 2 November 2016

Rouhani: Uingiliaji wa kigeni umeleta mgawanyiko Mashariki ya Kati


 Na Neema Dandida
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema matatizo yanayolikabili eneo hili la Mashariki ya Kati yamesababishwa na uingiliaji unaofanywa na nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo.
Katika mazungumzo yake na Demetris Syllouris, Rais wa Bunge la Cyprus hapo jana mjini Tehran, Rais Rouhani alisema, ili kuwa na mustakbali wenye mwangaza, maendeleo, usalama na ututivu, nchi za eneo hili sharti zishirikiane na kila moja itekeleze wajibu wake wa kimataifa.
Rais Hassan Rouhani ameelezea kusikitishwa kwake na namna mamilioni ya watu wasio na hatia katika nchi za Iraq, Syria, Yemen na Libya wanavyoendelea kukabiliwa na matatizo chungunzima kutokana na migawanyiko, uhasama na mapigano yaliyochochewa na nchi za Magharibi.


Mazungumzo ya Rais Hassan Rouhani na Demetris Syllouris, Rais wa Bunge la Cyprus Tehran
Kwengineko katika mazungumzo hayo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati ya Tehran na Nicosia na kubainisha kuwa, ushirikiano huo unaweza kuwa daraja ya kuunganisha Mashariki ya Kati na bara Ulaya pamoja na bara Afrika.
Kwa upande wake, Demetris Syllouris, Rais wa Bunge la Cyprus amesema kuchukuliwa hatua za kijeshi katika kuitafutia ufumbuzi migogoro inayolikabili eneo la Mashariki ya Kati, hakujakuwa na natija nyingine ghairi ya kuzidisha mizozo hiyo na kuibua mingine mipya. Amesema kuwa Cyprus iko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Iran katika nyuga za biashara, uchumi na utamaduni.
Rais wa Bunge la Cyprus ambaye aliwasili nchini Jumapili iliyopita kufuatia mwaliko wa Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu, Ali Larijani, amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa mbalimbali wa ngazi za juu wa serikali ya Tehran akiwemo Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran
Chanzo Pars Today

No comments:

Post a Comment