Rais Dk. John Magufuli
Rais
Dk. John Magufuli amesema amejitolea kuwa sadaka kwa Tanzania katika vita
dhidi ya mafisadi na kwamba akishindwa kufanya hivyo, hakuna sababu ya yeye
kuitwa rais.
Pia amesema wote
waliotumbuliwa majipu watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Akizungumza katika
hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika sehemu ya barabara ya Sakina hadi
Tengeru yenye urefu wa kilomita 14.1, itakayokuwa na njia nne, alisema
ataendelea kutumbua majipu kwa kuwa wanaonufaika na kudidimiza uchumi wa
nchi ni wachache.
“Tumeanza kuchukua
hatua ndogo ndogo, tunatumbua majipu. Mpaka sasa waliotumbuliwa si wengi kiasi
hicho, hawajafika hata 2,000. Juzi juzi nimesikia baadhi ya watu wameanza
kuwatetea wanaotumbuliwa, nasema hao wanaowatetea washindwe na walegee,”
alisema.
Hafla hiyo ilihudhuriwa
pia na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Makamu wa Pili
wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Butore, Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan Kusini,
James Wani Igga, Balozi wa Japan nchini na mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB).
Alisema wananchi
wa Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida na taabu kutokana na
wachache kufilisi mali na rasilimali za nchi.
“Ifike mahali mmoja
lazima ajitolee kufanya kazi hii. Mimi nimeamua kuwa sadaka kwa Tanzania,
lazima tufanye kazi ya kutumbua majipu na kuwaletea maendeleo wananchi.
“Nisipofanya hivyo,
hakuna sababu ya mimi kuitwa Rais. Hii nasema kwa dhati kabisa kutoka
moyoni mwangu, naomba Watanzania waniombee,”alisema.
Alisema kwa mfano yapo
mambo ya hovyo ambayo hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
imeisababishia serikali upotevu wa fedha za matumizi ya simu nje ya nchi husika
(roaming) kiasi cha Sh. bilioni 200.
Alisema watu wote
wanaojihusisha na ufisadi watafukuzwa na kufikishwa mahakamani mwishowe
kufungwa ili nao wakapate machungu.
“Hii nchi ilifika
mahali ikawa kama shamba la bibi vile,” alisema na kusisitiza kuwa katika
kuwaletea wananchi maendeleo hatafanya ubaguzi wowote kwa kuzingatia vyama,
dini, kabila ila atachapa kazi tu.
Alisema wananchi wa EAC
wanachohitaji si vyama ila kazi, maendeleo na maisha mazuri na si kuwafanya
wachache wawe wanafaidi kuliko wengine.
Awali,
alimpongeza Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kwamba ni
mtu mchapakazi.
“Nampongeza sana
Nassari, ni kijana safi anachotaka ni kazi na ameweza kuwaletea maendeleo
wananchi wa jimbo lake.
Sipendi kuwa mnafiki,
nampongeza sana Nassari. Ukimtazama usoni Nassari ni Chadema lakini kwa kweli
moyo wake uko CCM,” alisema na kufanya umati wa watu kulipuka kwa shangwe.
Mapema Rais Museveni
alisema: “Tukiwa tunazungumzia uchumi wa kisasa, Afrika hakuna umaskini, ina
utajiri mwingi wa raslimali isipokuwa inakosa maendeleo tu.
“Ardhi ipo, madini
yapo, lakini tunashindwa kuzitumia, hivyo tunakosa maendeleo, tunakosa elimu na
tuna afya duni,” alisema.
Aliwataka
wananchi kujikita katika kilimo cha kisasa badala ya kulimia tumbo peke yake. Museveni alisema
sekta ya kilimo, viwanda, huduma na ICT, ndizo zinazoweza kuleta maendeleo kwa nchi
za EAC.
Hata hivyo, alisema
shida ya Waafrika ni kulala na kwamba wanalala huku kukiwa kumekucha na
kusisitiza kuwa:
“Tukiamka sisi sote
tutakuwa na maendeleo kutokana na uzalishaji mkubwa utakaokuwapo,"
alisema.
Aliwaondoa
wananchi hofu ya kupatikana kwa soko pale aliposema jumuiya hiyo ina watu zaidi
ya milioni 160, hivyo idadi hiyo ni soko kubwa kwa bidhaa zitakazokuwa
zikizalishwa na wananchi.
Kwa upande wake, Rais
Kenyatta, alisema, viongozi wa jumuiya hiyo ndio waliofanya kazi ya kulala wakati
kumekucha.
Alisema kazi kubwa
waliyonayo wao ni kuwaletea maendeleo wananchi kwa kujenga miundombinu.
Aliwataka viongozi
wenzake kubadilika badala ya kuwa na maneno mengi na kwamba sasa wawe watu wa
kazi ambayo itawawezesha wananchi kupata maendeleo na kuyafurahia.
No comments:
Post a Comment