Friday, 4 March 2016

Mradi wa kutokomeza vifo vya wajawazito, watoto wazinduliwa.

Na Neema Dandida

 

 

 
 
 
 
 
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla amezindua mradi wa kutokomeza vifo vya wajawazito na watoto wachanga nchini katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

 Mradi huo unaofadhiliwa na taasisi ya Vodacom Foundation kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa ya Usaid, Path Finder na Touch Foundation, ulizinduliwa jana.
 Mradi huo unaojulikana kama `Moyo' awamu ya pili, umelenga kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha sekta ya afya nchini na adhma ya kutokomeza vifo vya wajawazito na watoto wachanga nchini.

 Dk. Kigwangalla alisema mradi huo unakwenda sambamba na malengo ya serikali ambayo imejipanga kuhakikisha matukio ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga vinavyojitokeza wakati wa kujifungua kutokana na ukosefu wa huduma za matibabu. vinatokomezwa.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao, alisema tangu mradi wa Moyo awamu ya kwanza uanze kutekelezwa mwaka 2009, umeandikisha wanawake zaidi ya 16,000 katika vituo vya afya na kuokoa maisha ya wajawazito na watoto zaidi ya 450.

 Alisema zipo changamoto kadhaa za baadhi ya wajawazito kutojifungua katika vituo vya afya, ambapo licha ya changamoto hizo mradi huo umewezesha mafunzo kwa wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii wanaopita kila kaya kutoa elimu ili kubadili mitazamo hasi ya baadhi ya akina mama kutofika kwenye vituo vya afya kupatiwa huduma za uzazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom Foundation, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, alisema pamoja na mafanikio ya kiafya yaliyopatikana kwa kukabiliana na ugonjwa wa fistula na huduma ya ujumbe mfupi wa maneno ya kuelimisha akina mama masuala ya uzazi kupitia mradi wa `Wazazi Nipendeni' kusaidia akina mama wengi, vile vile shughuli hiyo imekuwa ikiviwezesha vikundi vya kuweka na kukopa vya wanawake na kuwapatia mafunzo ya kuwawezesha kijikwamua  kiuchumi.

 Mkazi wa Sengerema, Lawrencia John, ambaye ni mmoja wa wanawake walionufaika,  aliupongeza mradi huo akisema ulimsaidia alipokuwa anajifungua mtoto wake wa kwanza.

 

No comments:

Post a Comment